MICHEZO… MASIKINI JUUKO NDIO BASI TENA KUTIMULIWA MSIMBAZI KISA…..

BEKI wa kati wa Simba, Juuko Murshid, mkataba wake na klabu hiyo unamalizika mwezi Desemba, lakini hivi karibuni viongozi wa timu hiyo wametofautiana kuhusiana na mchezaji huyo.

Baadhi ya viongozi wanataka beki huyo raia wa Uganda afungashiwe virago wakidai kuwa kwa sasa hana lolote klabuni hapo lakini wengine wanataka aendelee kubakia kwa kile walichodai kuwa bado ana mchango mkubwa katika kikosi cha timu hiyo na wengine wakihofia kusajiliwa na Yanga halafu akawatesa kama ilivyokuwa kwa Mrundi, Amissi Tambwe.

Msimu wa 2014/15, Simba ilimfungashia virago Tambwe na alipotua Yanga aligeuka kuwa mwiba mkali wa timu hiyo, jambo lilikuwa likiwaumiza vilivyo viongozi hao. Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa hali hiyo imewafanya viongozi hao kushindwa kufikia muafaka wa nini kifanyike juu ya beki huyo ambaye mwanzoni mwa msimu huu ilidaiwa kuwa Klabu ya Yanga ilikuwa ikimvizia ili iweze kumsajili.

“Mabadiliko katika kikosi chetu kipindi hiki cha dirisha dogo hayatakuwa makubwa sana mpaka sasa mchezaji
ambaye anatuvuruga vichwa ni Juuko Murshid ambaye mkataba wake unamalizika mwezi Desemba.

“Baadhi wanataka aondoke lakini wengine tunataka abakie kutokana na mchango wake kuwa bado unahitajika kikosini kwetu, ni kweli tuna mabeki wengi wazuri lakini baadhi yao si wazuri kama yeye, tukiachana naye katika kipindi hiki cha ushindani anaweza kutua Yanga na baadaye akaja kuwa kikwazo kikubwa kwetu kama ilivyokuwa kwa Tambwe pamoja na wachezaji wengine wengi tu.

“Hata hivyo, ngoja tusubiri tuone nini kitatokea kwani pia kabla ya kufanya maamuzi tutahitaji pia ripoti ya kocha,” kilisema chanzo hicho cha habari. Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Iddi Kajuna hakuwa tayari kusema chochote. Juuko tangu atue Simba mwaka 2014 amekuwa msaada mkubwa katika safu ya ulinzi ya timu hiyo licha ya msimu huu kukumbana na changamoto kubwa ya ushindani wa namba kutoka kwa Salim Mbonde ambaye kwa sasa ni majeruhi lakini pia kwa Mzimbabwe, Method Mwanjale.a

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*