KIMENUKA…NIYONZIMA AJITOA SIMBA KISA MASHABIKI…..

Haruna Niyonzima
HARUNA Niyonzima amejitoa kiaina Simba huku akiweka masharti ya kupewa wiki mbili ili aweze kujiweka fiti zaidi kwa kuboresha kiwango chake ili kuzima kelele za mashabiki wanaomlaumu kucheza chini ya kiwango.

Uamuzi huo wa Niyonzima raia wa Rwanda umekuja baada ya kuwepo kwa minong’ono mingi juu ya kiwango chake kushuka, na sasa amepania kukirejesha katika hali yake ya siku zote.

Niyonzima ametoa msimamo huo akiwa tayari ameichezea Simba michezo minne ya Ligi Kuu Bara huku akikosa mchezo mmoja pekee dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kutokana na kuugua Malaria.
Kiungo huyo ndiyo ameanza kuutumikia mkataba wake wa miaka miwili Simba aliyojiunga nayo msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Niyonzima alisema amezisikia lawama nyingi na za wazi kutoka kwa viongozi na mashabiki wa Simba wakimtuhumu kuwa kiwango chake kimeshuka kitu ambacho si sahihi.

Akisisitiza, Niyonzima alisema; “Ukweli ni kwamba, nilikosa maandalizi mazuri ya ‘Pre Season’ pamoja na wenzangu kutokana na kubanwa na baadhi ya majukumu nikiwa nyumbani Rwanda huku wao wakiwa kambini Afrika Kusini.
“Kiwango changu hakijashuka kama inavyoelezwa, ila tatizo lipo kwenye fitinesi ambayo nilichelewa kuitengeneza kwenye pre season na wenzangu.

“Leo (jana) nitakutana na kocha ili nimweleze hali halisi na nitamwomba aniandalie au nipewe programu maalumu ya mazoezi ya kuniongeza fitinesi ili niwe vizuri zaidi.
“Nataka iwe asubuhi nafanya kwenye gym na jioni kwenda kukimbia ufukweni, naamini nikiifanya vizuri programu hii, nitazima minong’ono yote ya mashabiki na viongozi wanaonituhumu.

“Baadhi ya viongozi wa Simba wamekuwa wakisema kuhusiana na mimi kiwango changu kimeshuka, kiukweli maneno hayo yananiumiza na kunikosesha amani, sasa nataka kuwaziba midomo,” alisema Niyonzima.
“Unajua sikwenda kambini Afrika Kusini, halafu nikarejea nchini siku moja kabla ya mechi na Rayon (SC ya Rwanda) kwenye sherehe ya Simba, hivyo nilicheza nikiwa sijafanya mazoezi.

“Niwaombe radhi mashabiki wa Simba, ninajua wanataka kuniona Niyonzima yule aliyekuwa anaichezea Yanga, ninaomba muda wa kujiweka sawa, ninawahakikishia watafurahi tu,” alimalizia Niyonzima.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*